Resource Details
Kupoteza mimba mara kwa mara kunaweza kuleta huzuni, hofu na maswali kwa mwanamke na mwenzi wake. Hali hii inaweza kuwa na sababu mbalimbali, na wakati mwingine chanzo hakipatikani hata baada ya uchunguzi. Si kosa la mwanamke pekee. Ni muhimu wenzi kupata ushauri wa mtaalamu wa afya na kufanyiwa uchunguzi unaofaa kabla au wakati wa kupanga ujauzito mwingine.
Takwimu zinaonyesha kuwa mimba kutoka ni changamoto muhimu ya afya ya uzazi. Nchini Tanzania, Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022 uliripoti kuwa asilimia 8 ya mimba zilizotajwa na washiriki ziliishia kwa mimba kutoka. Katika Afrika Mashariki, utafiti uliochapishwa mwaka 2026 ulionyesha kuwa asilimia 14.8 ya wanawake walioshiriki waliripoti kupoteza ujauzito. Kwa kiwango cha dunia, uchambuzi wa tafiti za kisayansi uliochapishwa katika jarida la The Lancet mwaka 2021 ulikadiria kuwa mimba milioni 23 hutoka kila mwaka, huku takribani asilimia 15.3 ya mimba zinazotambuliwa zikiishia kwa mimba kutoka. Utafiti huo pia ulibaini kuwa kila dakika moja, mimba za wanawake 44 hutoka. Takwimu hizi zinaonesha umuhimu wa kuongeza elimu kuhusu afya ya uzazi, kuondoa unyanyapaa na kuwahimiza wanawake kupata ushauri wa kitaalamu wanapokumbana na changamoto hii.